Breaking News

DONDOO MUHIMU KUELEKEA MTANANGE KATI YA AJAX VS MANCHESTER UNITED HUKO MJINI STOCKHOLM NCHINI SWEDEN

FRIENDS ARENA Mjini Stockholm Nchini Sweden kesho ndio Dimba la Fainali ya UEFA EUROPA LIGI kati ya Klabu ya Netherlands Ajax Amsterdam na Manchester United ya England.
Mbali ya kuwania Kombe pia Mshindi wa Fainali hii atatinga moja kwa moja Hatua ya Makundi ya UCL, UEFA CHAMPIONZ LIGI, na hilo ni muhimu mno kwa Man United kuliko Ajax kwani wao wamekosa nafasi hiyo baada ya kumaliza Nafasi ya 6 kwenye EPL, Ligi Kuu England, wakati Ajax wao wamepata Nafasi ya kucheza UCL kwa kumaliza Nafasi ya Pili kwenye Ligi ya kwao.
Hapo Kesho Ajax watakuwa wakiwania kutwaa Kombe la Ulaya kwa mara ya kwanza baada Miaka 22 wakati Man United wanalitaka Kombe pekee la Ulaya ambalo hawajawahi kulitwaa baada kutwaa mengine yote yaliyobakia.
Hii itakuwa ni mara ya 5 kwa Ajax na Man United kupambana kwenye Mashindano Barani Ulaya na kila Timu kushinda mara 2 ingawa mara zote hizo Man United kuibuka kidedea katika Mechi 2.
Mara ya kwanza Timu hizi zilikutana kwenye UEFA CUP Msimu wa 1976/77 na Ajax kushinda 1-0 Mechi ya kwanza huko kwao lakini Man United ikashinda 2-0 huko Old Trafford na kuibwaga Ajax.
Mara ya Pili ni Msimu wa 2012/13 kwenye UEFA EUROPA LIGI Raundi ya Mtoano ya Timu 32 ambayo Man United walishinda 2-0 huko Amsterdam kwa Bao za Ashley Young na Javier Hernández 'Chicharito' na Mechi ya Pili huko Old Trafford Ajax walishinda 2-1 na kutupwa nje ya Mashindano kwa Jumla ya Mabao 3-2.


JE WAJUA?
-MAN UNITED wanasaka kujumuika na Ajax, Bayern Munich, Chelsea na Juventus kwa kuwa Klabu pekee zilizonyakua Makombe yote ya UEFA huko Ulaya.
-Vikombe hivyo ni UEFA CHAMPIONZ LIGI, UEFA Cup Winners' Cup, UEFA Cup/UEFA EUROPA LIGI

Ajax, chini ya Kocha Peter Bosz, wanasaka kutwaa Kombe lao la kwanza tangu Bosi huyo atue hapo Mwezi Mei Mwaka Jana.
Nae Jose Mourinho, alianza kazi Man United mwanzoni mwa Msimu huu na tayari ashatia Kabatini Ngao ya Jamii na EFL CUP huko England na sasa analitaka Kombe hili ili Msimu ujao atinge UEFA CHAMPIONZ LIGI baada kumaliza Nafasi ya 6 kwenye EPL, LIGI KUU ENGLAND.

Hali za Timu
Ajax ni Timu inayocheza kwa kushambulia kwa haraka kwa mfumo wa kaunta ataki na Msimu huu kwenye Mashindano haya wamefunga Bao 24 wakati Man United wamepachika 23 katika Mechi 14.
Ajax, kikawaida, hutumia Mfumo wa 4-3-3 na Mtu 3 zao za Fowadi ni Kasper Dolberg, Bertrand Traore, ambae ni wa Mkopo kutoka Chelsea, na Amin Younes huku Fowadi wa Miaka 17, Justin Kluivert, Mwana wa Lejendari Patrick Kluivert, mara kwa mara akiingizwa kuongeza nguvu kwenye Wingi.
Kwa Man United, kumkosa Mkongwe Zlatan Ibrahimovic ambae ameumia na aliepiga Bao 5 kwenye Mashindano haya ni pigo lakini yupo Kinda Marcus Rashford ambae ni moto.
Pia kumkosa Ibrahimovic kunaweza kumfanya Jose Mourinho akabadili Mfumo kutoka ule wa kawaida yao wa 4-2-3-1.
Nguvu kubwa ya Ajax ipo kwenye Kiungo chao na hasa Davy Klassen na Lasse Schone na endapo Ander Herrera na Paul Pogba wataibuka juu yao, Difensi ya Ajax, hasa Masentahafu Davinson Sanchez na Nick Viergever, si imara kiasi hicho kwani huwa mchecheto kwenye presha na wao na Kipa wao Onana hufanya makosa mengi kwenye hali hiyo.

VIKOSI VINATARAJIWA KUWA:
AJAX: Onana; Tete, De Ligt, Sanchez, Veltman; Klaassen, Schone, Ziyech; Traore, Dolberg, Younes

MAN UNITED: Romero; Valencia, Blind, Jones, Darmian; Herrera, Fellaini, Pogba; Lingard, Rashford, Mkhitaryan
REFA: Damir Skomina (Slovenia)

No comments