AS ROMA YAIZUIA JUVENTUS KUTANGAZA UBINGWA MAPEMA SERIE A
Juventus imekosa nafasi ya kutwaa Ubingwa wao wa Serie A wa 6 mfululizo mapema kabla Ligi hiyo kuu ya Italy kwisha baada Jana kudundwa Bao 3-1 Ugenini na Timu ya Pili AS Roma.
Hata hivyo, Juve wanabaki kileleni mwa Serie A wakiwa Pointi 4 mbele ya Roma huku Mechi zikibaki 2 na Jumapili ijayo, wakiwa kwao Juventus Stadium Jijini Turin, wana nafasi nyingine ya kuwa Mabingwa ikiwa wataifunga Crotone.
Kabla ya hapo, Jumatano Usiku, wanapambana na SS Lazio kwenye Fainali ya Coppa Italia.
Jana Juve walitangulia kuifunga Roma kupitia Mario Lemina lakini Bao za Daniele de Rossi, Stephan El Shaarawy na Radja Nainggolan ziliipa Roma ushindi wa 3-1 na kuweka hai matumaini yao finyu ya kuwa Mabingwa.
Juve, chini ya Kocha Massimiliano Allegri, wanahitaji Pointi 1 tu ili kutwaa Ubingwa wa Serie A na kuweka Rekodi ya kuwa Timu pekee kutwaa Ubingwa mara 6 mfululizo katika Historia ya Italy.
Lakini pia Juve wanaweza kutwaa Ubingwa Jumamosi hii bila wao kucheza ikiwa tu Roma itafungwa Ugenini na Chievo na Napoli, wakiwa Nyumbani, kushindwa kuifunga Fiorentina.
Kwa wakati huo, Juve, ikiwa Jumatano watatwaa Coppa Italia, watajijua kama wako mbioni kutwaa Trebo Msimu huu kwani pia wanacheza Fainali ya UEFA CHAMPIONZ na Real Madrid hapo Juni 3 huko Cardiff, Wales.

No comments