AHMAD AHMAD ASHINDA URAIS WA SHIRIKISHO LA MPIRA AFRICA (CAF)
Ahmad Ahmad leo ameibuka kidedea na kumbwaga mpinzani wake, Issa Hayatou katika kinyang’anyiro cha Urais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
Ahmad ambaye ni Rais wa chama cha soka cha Madagascar amembwaga Hayatou ambaye amekalia kiti hicho kwa mda mrefu baada ya kupata kura 34 dhidi ya 20 za Hayatou.
Matokeo hayo yanahitimisha miaka 29 ya utawala wa Hayatou, mwenye miaka 70 kama kiongozi wa juu wa Soka Barani Afrika tangu mwaka 1988.
Alianza kutawala tangu March 10, 1988 alikuwa anaifukuzia rekodi ya kuendelea kusalia madarakani kwa awamu ya nane mfululizo.
Uchaguzi huo umefanyika leo baada ya mkutano mkuu wa 39 huko Mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Wakati huohuo, CAF imeridhia na kupitisha ombi la Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFA) la kuwa mwanachama rasmi wa CAF.
Zanzibar sasa inakuwa nchi ya 55 mwanachama wa kujitegemea wa CAF ambapo awali ilikuwa inaunganisha na Tanzania Bara chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kupelekea kukosa haki za kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF na FIFA kama nchi inayojitegemea.
No comments