Breaking News

KUELEKEA MCHEZO WA NGAO YA HISANI MAKOCHA WA SIMBA NA YANGA WATAMBIANA

Zikiwa zimesalia siku kadhaa kabla ya kuchezwa kwa mtanange wa Ufunguzi wa ligi kuu Tanzania bara makocha wa vilabu vitavyo shiriki mtanange huo wamefunguka na kuweka bayana namna mchezo huo utakavyokua mgumu kwa kila upande na hivyo kutotegemea timu yoyote kufungwa kirahisi hivyo atakae fungwa ni bahati tu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti makocha hao walisema bahati ni jambo linaloibeba timu, huku kila mmoja akiomba Jumatano bahati hiyo imuangukie.

Omog alisema amekamilisha mazoezi yote aliyoyaandaa kwa ajili ya mchezo huo na sasa anachosubiri ni muda na siku ya mechi ifike.
"Tumefanya kila kitu muhimu kinachotakiwa kuelekea mchezo wetu dhidi ya Yanga, wachezaji wanajua umuhimu na changamoto ya mechi hiyo, tunaomba Mungu atupe nguvu na kuwa upande wetu siku ya Jumatano," alisema Mcameroon huyo.
Aliongeza kuwa juzi kabla ya kuivaa Mlandege kikosi chake kilifanya mazoezi makali asubuhi na ndiyo sababu wachezaji wake hawakuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo wa kirafiki uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.

Mzambia Lwandamina alisema kuwa amewaambia wachezaji wake wasiwe na presha yoyote na kusahau matokeo ya mechi iliyopita ambayo walilala mabao 2-1.
"Huu ni msimu mpya, tunahitaji kufungua ukurasa mpya, nimewapa mazoezi na mbinu zote muhimu kuwakabili Simba, kikubwa tunahitaji kuamka salama na kwenda kuonyesha tulichojifunza uwanjani," alisema kocha huyo wa zamani wa Zesco.
Aliongeza kuwa amewaandaa wachezaji wake kutobweteka katika mchezo huo na pia wasitishwe na ukubwa wa majina ya baadhi ya nyota walioko Simba ambao wamesajiliwa msimu huu kutoka ndani na nje ya nchi.
"Tunawafahamu na wao wanatufahamu, naamini atakayetumia vyema nafasi za kufunga katika mechi hiyo ndiye ataibuka mshindi, ni mechi yenye ushindani na itakayotupa mwelekeo wa msimu mpya," Lwandamina aliongeza.
Mechi hiyo ya kuwania Ngao ya Jamii inatarajiwa kupigwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na timu zote mbili zimeweka kambi Zanzibar.

No comments